Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Bunge; Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Bi. Jenista Mhagama akiwa na Naibu wake Dkt. Abdallah Posi
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Bi. Jennista Mhagama, amesema hayo leo wakati akitoa ripoti ya matokeo ya utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi kwa mwaka 2014, utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu - NBS.
Ripoti hiyo inaonesha takribani nguvu kazi iliyopo nchini ni watu milioni 25 na zaidi ya watu milioni 17 wakiwa wanatumia muda wao mwingi bila shughuli huku wakilalamikia huduma mbovu kutoka kwa serikali wakati na wao wanatakiwa kuwa kati ya watu wanaotakiwa kuboresha hali hiyo.
Waziri Mhagama amesema kuwa kutokana na idadi kubwa ya watu kutokufanyakazi kuna haja ya kurejesha sheria ya nguvu kwa ajili ya kuzuia wazururaji na wanaokaa bila shughuli ya msingi ya kufanya.
Kwa mujibu wa Waziri Mhagama, amesema idadi hiyo ni kubwa sana na inaashiria ni kwa kiwango gani nguvukazi kubwa ya nchi haitumiki katika uzalishaji na hubakia kulalamikia huduma mbovu kutoka serikalini badala ya wao kuwa sehemu ya uzalishaji.
Kauli ya Waziri Mhagama imekuja huku sehemu ya maudhui ya ripoti hiyo yakionesha kupungua kidogo kwa kiwango cha ukosefu wa ajira nchini kutoka asilimia 11.7 ilivyokuwa mwaka 2006/7 mpaka asilimia 10.3 mwaka 2014/15.