Jumanne , 12th Apr , 2016

Ligi kuu ya Soka Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea hapo kesho kwa kupigwa michezo miwili ya viporo ambapo Yanga itashuka Uwanja wa Taifa kuikaribisha Mwadui huku Azam FC ikiwa ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Manungu Mkoani morogoro.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Yanga Jerry Muro amesema, Mwadui ni wazuri japo Kocha wao anajua kuongea na kama angekuwa ndiye mchezaji wangehesabu wameshafungwa katika mchezo huo.

Muro amesema, wanaamini mchezo huo ambao ni kiporo watafanikiwa kuibuka na pointi tatau kwani kikosi cha yanga kipo vizuri na kipo tayari kwa ajili ya ushindi.

Kwa upande wake Afisa habari wa Azam FC Jaffery Iddy Maganga ambao wanashuka hapo kesho Uwanja wa Manungu Mkoani Morogoro amesema, katika mchezo huo watamkosa mlinzi wao Serge Paschal Wawa ambaye aliumia katika mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Esperance lakini katika michezo ijayo atakuwepo Uwanjani.

Azam FC imeondoka hii leo kuelekea Mkoani Morogoro ambapo itafikia Morogoro Mjini na asubuhi ya hapo kesho wataanza safari ya kuelekea Manungu kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo.