Kundi la wachezaji lilifika makao makuu ya klabu, mapema asubuhi ya leo mjini Tanga wakiwa na mabango yenye kuwasilisha kilio chao cha kudai mishahara.
Wachezaji hao hawakwenda kufanya mazoezi leo asubuhi huku ikiwa haijulikani msimamo wao huo utaendelea kwa muda gani.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Coastal Union, Oscar Assenga amesema amesikia taarifa hizo, lakini hazijui vyema kwa sababu yupo nje ya Tanga.
Mwenyekiti wa sasa wa Coastal Union, Dk Ahmed Twaha amesema kwamba watakutana na wachezaji leo jioni na baada ya hapo watatoa taarifa ya mustakabali wa tatizo hilo.
Coastal Union inashika nafasi ya 14 kwenye Ligi Kuu yenye timu 16, ikiwa na pointi 16 baada ya kucheza mechi 20.
Coastal Union wanawazidi kwa wastani wa mabao ndugu zao, African Sports walio nafasi ya 15 wakiwa na pointi 16 pia, baada ya kucheza mechi 20, wakati JKT Ruvu yenye pointi 15 za mechi 20 ndiyo inashika mkia.