Alhamisi , 24th Dec , 2015

Wachezaji wa kitanzania wametakiwa kutumia vizuri nafasi wanazozipata za kucheza Soka la Kimataifa ili kuweza kujikuza zaidi katika Soka.

Mshambuliaji wa Kimataifa ambaye alikuwa akiitumikia Klabu ya Simba na hivi sasa anaitumikia Klabu ya Royal Eagles ya nchini Africa Kusini Uhuru Suleiman amesema, Afrika kusini nafasi zipo nyingi na hata kwa nchi zote Duniani ambazo zinacheza Mpira wa kueleweka lakini wachezaji wanatakiwa kujiandaa.

Uhuru amesema, timu za nje zinajali wachezaji na mchezaji wa Kitanzania atakapoitwa kuzitumikia timu hizo ni lazima awe amejiandaa kwa sababu mchezaji anapoitwa nafasi inakuwepo lakini anatakiwa aipiganie kwa kujiandaa kwa ushindani kwani mpira wa Afrika kusini na nchi nyingine ni wanguvu sana hivyo mchezaji anatakiwa awe amejijenga kiakili na awe tayari kwa ajili ya kufanya kazi ya mpira.

Uhuru amewataka wachezaji wa Kitanzania kutunza miili yao pamoja na kujifunza Lugha ili kuweza kuelewana na uongozi pamoja na wachezaji wenzake kwani nafasi zipo kwa Watanzania na wameshaanza kujitangaza.

Uhuru amesema, ni muda wa kutoka kwa wachezaji wa Kitanzania na kuna njia kwani imeshafahamika kuwa Tanzania kunawachezaji hivyo mawakala watakuja kwa ajili ya kutafuta wachezaji na wachezaji pia wanatakiwa na nafasi zipo hivyo ni kwa wachezaji kuwa tayari na kuangalia nini wanaenda kukifanya.

Uhuru amesema, wachezaji wanaohitaji kucheza Soka la Kimataifa wasisite kushirikiana na wachezaji mbalimbali ambao wameshatoka ili kuongeza idadi ya wachezaji wa kimataifa pamoja na kuweka ushindani kwa wachezaji wa kitanzania ambao wanacheza Soka la Kimataifa.