Jumanne , 28th Jul , 2015

Robo fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na kati, Kombe la Kagame inaanza kutimua vumbi hii leo kwa kuzikutanisha timu ya APR na Khartoum ukifuatiwa na Gor Mahia watakaocheza dhidi ya Malakia uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Afisa habari wa Shirikisho la Soka nchini TFF, Baraka Kizuguto amesema, mchezo wa kwanza ambapo ni kati ya APR na Khartoum utaanza saa nane kasorobo huku ule wa pili utakaowakutanisha Gor Mahia dhidi ya Malakia ukianza saa 10 na robo ili kuzipa timu nafasi endapo zikitoka sare kuweza kwenda katika hatua ya matuta.

Kizuguto amesema, robo fainali ya pili itafanyika hapo kesho kwa kuzikutanisha wenyeji Yanga na Azam FC ukitanguliwa na mchezo kati KCC dhidi ya Al Shandy uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam huku nusu Fainali ikitazamiwa kuchezwa siku ya Ijumaa na fainali ikichezwa Jumapili ikitanguliwa na mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu.