Jumatatu , 3rd Mar , 2025

Rais wa Marekani Donald Trump ametia saini agizo la kukifanya Kiingereza kuwa lugha rasmi ya Marekani.

Amri hiyo inabatilisha sera inayovitaka vyombo hivyo kutoa usaidizi wa lugha kwa wasiozungumza Kiingereza, iliyotiwa saini na rais wa zamani Bill Clinton mwaka 2000.

Hii ni mara ya kwanza kwa Marekani kuteua lugha fulani kuwa lugha yake rasmi katika ngazi ya shirikisho tangu nchi hiyo ianzishwe karibu miaka 250 iliyopita.

Agizo hilo limweka wazi kuwa mashirika hayo hayahitajiki kubadilisha, kuondoa au kuacha kutoa usaidizi wowote wa lugha ambao tayari inatoa.

Takribani wakazi milioni 68 kati ya milioni 340 nchini humo wanazungumza lugha nyingine isiyokuwa Kiingereza, kulingana na Ofisi ya Sensa ya Marekani.

Hii inajumuisha zaidi ya lugha 160 za Wenyeji wa Marekani.

Kihispania, Kichina na Kiarabu ni miongoni mwa lugha zinazozungumzwa zaidi baada ya Kiingereza, kulingana na Ofisi ya Sensa.

Wanachama wa Republican hapo awali walijaribu kukifanya Kiingereza kiteuliwe kuwa lugha rasmi ya Marekani, lakini juhudi hiyo haikufaulu mwaka 2021.

Waliopinga juhudi hiyo walisema lugha rasmi sio lazima iwe lugha yenye idadi kubwa ya watu wanaozungumza. Pia walisema kukifanya Kiingereza kuwa lugha rasmi kunaweza kuchochea ubaguzi dhidi ya wasiozungumza Kiingereza.
Takriban nchi 180 duniani zina lugha rasmi ya kitaifa, na nchi nyingi zinatambua lugha rasmi zaidi ya moja. Na nchi nyingine hazina lugha rasmi, ikiwa ni pamoja na Uingereza.