Jumatatu , 3rd Mar , 2025

Afisa wa ngazi ya juu wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) ameonya katika barua pepe siku ya Jumapili, kwamba hatua ya serikali ya Trump ya kulivunja shirika hilo itasababisha vifo visivyo vya lazima.

Barua pepe hiyo kwa wafanyakazi wake ilikuja ndani ya dakika 30 tu baadaye kusema amepewa likizo.

Nicholas Enrich, kaimu msimamizi msaidizi wa USAID katika masuala ya afya duniani, amesema katika risala ya kurasa saba iliyoonekana na Reuters, "uongozi wa kisiasa, umefanya iwe vigumu kutoa msaada wa kibinadamu wa kuokoa maisha duniani kote.”

Dakika ishirini baadaye, Enrich alituma barua pepe nyingine, ambayo pia imeonekana na Reuters, akisema "nimepokea taarifa kwamba nimepewa likizo."

Chanzo kinachofahamu suala hilo kimesema uamuzi wa kumwondoa Enrich kazini ulifanywa Jumatano, kabla ya kutuma barua pepe yake.

Misaada ya USAID ambayo imezuiliwa ni pamoja na juhudi za kusaidia kudhibiti mlipuko mbaya wa Ebola nchini Uganda ambao umeua watu wawili na kuambukiza 10, Enrich alisema katika risala yake.
"Hili bila shaka litasababisha vifo vinavyoweza kuzuilika," ameandika Enrich kwenye risala, ambayo iliandikwa Februari 28 na kuwekwa hadharani Jumapili mchana.
Utawala wa Trump ulitangaza wiki iliyopita inazuia karibu misaada 10,000 ya kigeni na kandarasi zenye thamani ya karibu dola bilioni 60, na hivyo kukatiza takriban 90% ya kazi ya kimataifa ya USAID.