Jumatano , 22nd Jul , 2015

Upungufu wa madawati katika shule mbalimbali za msingi nchini Tanzania imekuwa kikwazo kikubwa katika kusaidia wanafunzi kufikia malengo yao licha ya jitihada zinazofanywa na taasisi mbalimbali katika kupungunza changamoto hiyo.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Kaimu mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu (TEA), Bw.Joel Laurent wakati wa kukabidhi madawati 1,500 kwa shule za msingi 15 zilizopo jijini Dar es salaam katika kukabiliana na tatizo la upungufu wa madawati ambapo amesema zaidi ya wanafunzi 5000 wanatarajiwa kunufaika na madawati hayo ambayo yana thamani ya shilingi milioni 130.

Bw Laurent amesema kuwa tathmini ya mwaka 2013 Tanzania ina upungufu wa madawati zaidi ya milioni moja na hivyo ni jukumu la kila mdau kuunga mkono juhudi hizo ili kuondoa tatizo hilo kote nchini.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mahusiano wa benki ya KCB Bi Christina Manyenye amesema wamekuwa wakishiriki katika kuchangia madawati lengo likiwa ni kusaidia kuinua elimu kupitia mfuko wa elimu ulioundwa na taasisi hiyo ambapo kwa mwaka huu wamechangia madawati 1000 yenye thamani ya shilingi milioni 80.

Akifafanua Bi. Lupembe amesema shule zitakazonufaika ni Tabata, Buguruni, Mbagala, Kiburugwa, Makamba, Kilungule, Charambe, Kiimbwa na Wandege, Ukuni , Madenge, Kisukuru, Kimwammi na Mabatini.