Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Mathew Akrama wa Mwanza, Yanga SC walitawala zaidi kipindi cha kwanza na kupoteza nafasi kadhaa za kufunga mabao.
Yanga SC walipoteza nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 29, baada ya shuti la mpira wa adhabu la beki wake wa kulia, Juma Abdul kupanguliwa vizuri na kipa Jeremiah Kisubi wa Ndanda.
Yanga SC walisukuma shambulizi kali langoni mwa Ndanda dakika ya 42 na kuzua kizaaa, kabla ya beki mmoja kuokoa mpira uliokuwa unaelekea nyavuni.
Kipindi cha pili, Yanga SC walirudi kwa kasi ile ile ya mashambulizi na kufanikiwa kupata penalti dakika ya 47, baada ya beki wa Ndanda, Paul Ngalema kumuangusha winga Simon Msuva kwenye boksi.
Hata hivyo, mshambuliaji Mrundi Amissi Tambwe akaenda kugongesha mwamba wa juu mkwaju wake na ingawa alijaribu kuucheza tena uliporudi uwanjani, hakufanikiwa.
Dakika ya 60 Deus Kaseke aliyekuwa akienda kumsabahi Kisubi alikwatuliwa na Braison Raphael na kusababisha penati iliyopigwa na mlinzi Kelvin Yondan aliyeukwamisha mpira wavuni na kuiandikia Yanga bao pekee.
Kwa ushindi huo Yanga imerejea kileleni ikiwa na pointi 36 sawa na Azam ila inaizidi kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 30.

