Jumatatu , 2nd Feb , 2015

Klabu ya Yanga imeliomba Shirikisho la Soka nchini Tanzania TFF, kusogeza mchezo wao mbele dhidi ya Mtibwa uliotarajiwa kuchezwa uwanja wa Taifa Jumamosi wiki hii baada ya kumaliza mechi dhidi ya Coastal Union itakayochezwa Jumatano jijini Tanga.

Akizungumza na East Africa Radio, Afisa Habari wa Klabu ya Yanga, Jerry Muro amesema wameamua kuomba mchezo huo kusogezwa mbele ili kuweza kupata nafasi ya kujiandaa na michuano ya Kombe la Shirikisho inayotarajiwa kuanza Februari 14 mwaka huu katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam ambapo Yanga wataanza na timu ya BDF ya nchini Botswana.

Muro amesema, hivi sasa wapo katika maandalizi kwa ajili ya kuanza kambi kwa ajili ya michuano hiyo ambayo sio kuiwakilisha Yanga pekee bali wanaiwakilisha nchi kwa ujumla na wanaamini kutokana na maandalizi watakayoyafanya wataiwakilisha nchi vizuri katika michuano hiyo.