Jumamosi , 12th Mar , 2016

Mholanzi wa Yanga SC, hii leo ametumia wembe ulioinyoa Simba baada ya kukianzisha kikosi ambacho alikitumia kwenye mechi dhidi ya mahasimu, wao Simba Februari 20, mwaka huu na kuiua timu ya APR jioni ya leo katika uwanja wa Amahoro, jijini Kigali.

Kikosi cha Yanga kilichoivaa Simba wiki tatu zilizopita ndiyo kimeivaa APR hii leo.

Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Soka Tanzania bara ambao ni wawakilishi wa Tanzania bara katika ngarambe za michuano ya klabu bingwa barani Afrika timu ya Yanga wamefanikiwa kujiweka katika mazingaira mujarabu baada ya kuibuka na ushindi wa bao 2-1 katika mchezo ambao ulikuwa wa taratibu huku kila timu ikijihami muda wote wa mchezo huo uliopigwa katika dimba la taifa la Amahoro mjini Kigali, Rwanda dhidi ya wenyeji, maafande wa jeshi la Rwanda timu ya APR ukiwa ni mtanange wa kwanza wa Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.

Maajabu ya mchezo huo ambao hii leo kocha Mholanzi wa Yanga Hans Van Pluijm aliyafanya ni pamoja na kutumia idadi ya wachezaji 10 kati ya 11 aliowaanzisha akiwafunga 2-0 watani zao Simba katika Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara mchezo uliopigwa katika dimba la taifa, jijini Dar es Salaam,

Katika kikosi hicho ambacho hii leo kilijipatia bao la kuongoza katika dakika ya 19 kupitia mkwaju mkali wa faulo ya moja kwa moja iliyopigwa na beki kisiki wa upande wa kulia wa Yanga Juma Abdul kocha aliwaanzisha kwa pamoja washambuliaji pacha Amissi Tambwe wa Burundi na Mzimbabwe Donald Ngoma huku akikipangua kidogo kikosi kwa kumpumzisha kiraka Mbuyu Twite na kumrejesha beki katili Kevin Yondan ambaye Februari 20 alikuwa anatumikia adhabu ya kadi nyekundu.

Goli la pili la Yanga katika mchezo huo lilifungwa na kiungo aliye katika kiwango bora kwa sasa Mzimbabwe Thaban Kamusoko kunako dakika ya 75 kipindi cha pili baada ya kuuwahi mpira ulipigwa na winga mwenye kasi Simon Msuva aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya mshambuliaji Amis Tambwe na Kamusoko kuachia mkwaju mwepesi ambao ulimshinda kipa wa APR kwa kumbabatiza kifuani na kujaa katika nyavu ndogo.

Watu wakiamini kama mpira huo utaisha kwa matokeo ya mabao 2-0 mambo yakabadilika kunako dakika ya 90 baada ya mshambuliaji Frank Sibomana kuipatia bao APR na hivyo kufanya mchezo huo kumalizika kwa matokeo ya bao 2-1.

Matokeo hayo yameipa nafasi Yanga kujiweka katika mazingira mazuri ya mchezo wa marudiano utakaopigwa wiki mbili zijazo katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam kwani sasa Yanga itahitaji sare ya aina yoyote ili kujihakikishia kuvuka raundi hiyo huku wenyeji wao APR wakihitaji ushindi wa si chini ya mabao 2-0 ili kusonga mbele na kuwaondosha Yanga katika michuano hiyo.