Baadhi ya wachezaji wa mpira wa wavu wakichuana katika moja ya michezo yao ya ligi ya mkoa.
Chama cha Mpira wa Wavu Mkoa wa Dar es Salaam kinataraji kuendelea na mipango yake ya kimashindano mwezi ujao wakati watakapoendesha ligi ya mpira wa wavu kwa vyuo vikuu itakayoanza April 2 mwaka huu na baadae kufuatiwa na ligi ndefu ya mkoa itakayoanza April 16.
Katibu mkuu wa chama cha Mpira wa Wavu mkoa wa Dar es Salaam DAREVA Yusuph Mkarambati amesema tayari wameshaanza maandalizi ya mashindano ya vyuo vikuu ambayo safari hii kwa mara ya kwanza yatakuwa yakifanyika katika viwanja vya vyuo vyote shiriki vitakavyoshiriki mashindano hayo.
Mkarambati amesema wamefikia uamuzi huo wakupeleka mashindano hayo katika vyuo husika ama shiriki kwa lengo la kuutangaza mchezo kwa watu wengine hasa jumuiya ya wanavyuo hivyo na kuwavutia kuupenda mchezo huo na pia kubwa kuongeza ushindani kwa timu shiriki kwakuwa kila timu itakuwa ikicheza vizuri ili iweze kushinda mchezo wa nyumbani mbele ya mashabiki wake.
Akimalizia Mkarambati amesema ligi hiyo ya vyuo vikuu itakayoanza April 2 mwaka huu itakuwa ni ligi fupi yenye timu nane za vyuo vikuu kutoka jijini Dar es Salaam ambayo baadae sasa itafuatiwa na ligi ndefu ya klabu bingwa ya mkoa itakayoanza kuanzia April 16 mwaka huu hadi mwezi August mwaa huu ikishirikisha vilabu takribani 12 vitakavyochuana kusaka ubingwa wa mkoa huku pia wachezaji wakiwania nafasi yakuteuliwa kuunda kikosi cha timu ya mkoa itakayoshiriki mashindano mbalimbali ya ndani na nje katika medani ya kitaifa na kimataifa kama Ubingwa wa taifa na mashindano ya majiji.