Alhamisi , 16th Mar , 2017

Samir Nasri amemwita mshambuliaji wa Leicester City Jamie Vardy "Mwongo", kufuatia kuhusika kwake kumsababishia kiungo huyo wa Sevilla kutolewa kwa kadi nyekundu, kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya, Jumanne.

Jinsi tukio lilivyokuwa

Nasri, ambaye anacheza kwa mkopo kwenye timu ya Sevilla ya Hispania kutoka Manchester City ya Uingereza, alipewa kadi nyekundu katika dakika ya 74, kwa kumpiga kichwa Vardy baada ya wachezaji hao, kugombana walipokuwa bila ya mpira.

Leicester iliwatoa mabingwa hao, wa Europa League wa msimu uliopita, kwa jumla ya mabao 3-2, kwenye mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa King Power, na mbweha hao kutinga robo fainali ya ligi ya mabingwa Barani Ulaya kwa mara ya kwanza.

"Kwa mimi yeye ni mwongo kwa sababu kama angekuwa mchezaji wa kigeni, nyinyi waandishi wa Uingereza, mngesema kuwa ni mwongo, kwa mimi yeye (Vardy) ni mwongo," alisema kiungo huyo wa zamani wa Arsenal.