Ijumaa , 24th Jun , 2016

Kocha wa timu ya Taifa ya vijana ya Tanzania Serengeti Boys Bakary Shime amesema, wapo tayari kwa mchezo wa awali wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa kwa vijana dhidi ya Shelisheli jumapili Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kocha wa Serengeti Boys Bakary Shime akitoa maelekezo wakati wa mazoezi kwa vijana wake Uwanja wa Karume jijini Dar es salaam

Shime amesema, anaamini mchezo utakuwa ni mgumu kutokana na kila timu kuhitaji ushindi ili kuweza kusonga mbele lakini anaamini kwa maandalizi ya kikosi chake wataibuka na ushindi.

Kwa upande mwingine Shime amewataka wadau wa michezo kujitokeza kwa ajili ya kuweza kuwasaidia vijana ambao wanawakilisha nchi katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Shime amesema, licha ya Airtel ambao wanahusika kwa kiasi kikubwa katika kukuza vipaji vya soka kwa vijana lakini wanatakiwa kuendeleza kuwapasapoti vijana hao hata wanapokuwa timu ya Taifa ili kuweza kuwaendeleza zaidi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Beatrice Singanno amesema, wanajivunia kuwa na vijana ambao wamewakuza na hivi sasa wanaiwakilisha nchi vizuri katika mashindano mbalimbali.

Beatrice amesema, wanaamini na Serengeti Boys pamoja na uongozi wao mzima kwani maandalizi mazuri kwa timu yanachangia ushindi kwa asilimia kubwa.