Waziri wa Habari , Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye akipokea nakala ya barua ya malalamiko ya Simba kwa TFF kutoka kwa Mkuu wa Idara ya Habari ya Simba Haji Manara
Barua hiyo ya Simba kwenda kwa TFF na kopi kwa Nape, inawalalamikia pia wachezaji wawili nyota wa Yanga, Donald Ngoma na Amissi Tambwe kutokana na vitendo vyao vya nidhamu huku shirikisho hilo lilionekana kuvifumbia macho.
Sehemu ya barua hiyo, inaeleza Mkuu wa kitengo cha mawasiliano cha Yanga, Jerry Muro kutumia lugha za kibaguzi pamoja na kuonyesha dharau kwa kutoa kauli ambazo si za kiungwana.
Simba inawatuhumu Tambwe kwa kumvuta korodani Juuko Murshid na Ngoma kumpiga kichwa kwa makusudi beki Hassan Kessy lakini kamati ya nidhamu chini ya TFF, kamwe haijawahi kukaa na kusikiliza, badala yake inaonekana kuziba masikio.
Manara alikabidhisha barua hiyo TFF mbele ya waandishi wa habari ili kuonyesha kuwa kweli suala hilo limefika. Lakini akafanya hivyo pia kwa Waziri Nape.
Pia barua hiyo ya Simba iliyosainiwa na Katibu Mkuu wake, Amos Gahumeni, imetaka TFF kuhakikisha Azam FC, Yanga nazo zinacheza mechi zake mbili za viporo ili kuepusha suala la upangaji matokeo mwishoni.
Wakati huo huo uongozi wa klabu hiyo umemwandikia barua kiungo wa timu hiyo Abdi Banda ambaye hivi karibuni aliripotiwa na kocha wake kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu wakati timu hiyo ikiwa jijini Tanga ilipokwenda kucheza na Coastal Unio.
Mkuu wa idara ya habari ya timu hiyo Haji Manara amesema Banda anatakiwa kutoa maelezo ya utetezi wake kabla ya kamati ya nidhamu ya timu hiyo kuketi na kufanya maamuzi ya mwisho.
Miongoni mwa tuhuma zinazomkabili Abdi Banda ni pamoja na kitendo cha kugomea maagizo ya kocha wake Jackson Mayanja aliyemtaka kupasha misuli ili aweze kuingia kiwanjani kuchukua nafasi ya beki kisiki wa timu hiyo Mohamed Hussein Tshabalala wakati mchezo kati ya timu hiyo dhidi ya wagosi wa kaya Coastal Union uliopigwa katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga na Simba kuibuka na ushindi wa bao 2-0.
Tuhuma nyingine ambayo Manara ameiita ni kubwa zaidi ni ile ya mchezaji huyo kugomea ama kutovaa sare yenye nembo ya mdhamini wa klabu hiyo kitu ambacho kwa klabu ni kosa kubwa na linaweza kuhatarisha udhamini wa klabu hiyo ama kuleta mgongano wa kimaslahi baina ya pande mbili hizo.
Tayari Banda alishapokea barua yake tangu jana na sasa amepewa muda wa siku mbili tangu kupokea barua hiyo na ndipo awasilishe utetezi wake kabla ya kamati ya nidhamu haijaketi na kutoa maamuzi ya sakata hilo.
Ikumbukwe ni wiki moja tu imepita tangu klabu hio ilipotangaza kumfungia kwa mwezi mmoja na kumlipa nusu mshahara beki wake kisiki wa kati kinda Hassan Isihaka kufuatia utovu wa nidhamu akimtolea lugha chafu kocha wake wakati wa mchezo wa kombe la shirikisho Tanzania baina ya timu hiyo na Singida United ulioishia kwa Simba kushinda bao 5-1.
Tangu kutua katika klabu ya Simba kocha Mayanja amekuwa ni kocha mwenye imani kubwa na suala la nidhamu ndani na nje ya uwanja kwa wachezaji wote na mara nyingi amekuwa mtu wa kazi na hana masihara katika kazi yake.