Razak Siwa aipaisha Dodoma Jiji

Jumamosi , 17th Jul , 2021

Kocha wa magoli kipa wa klabu ya Yanga, Razak Siwa ameipaisha klabu ya Dodoma Jiji na kusema ni timu nzuri hivyo hawana budi kupambana ili kusaka alama tatu kwenye mchezo wa VPL utakaowakutanisha wawili hao kesho Julai 18, 2021 kwenye dimba la Jamhuri Jijini Dodoma.

Kipa wa magolikipa wa kikosi cha Yanga, Mkenya Razak Siwa (wa kwanza kushoto) akiwa na Said Ntibazonkiza na Metacha Mnata baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa Dodoma wakitokea Jijini Dar es Salaam.

Kocha Siwa amesema; “Tumejiandaa vizuri sana kwa mechi hiyo ya mwisho wa ligi na Dodoma Jiji, tutapamabana kupata alama hizo tatu ili tumalize vizur”.

“Dodoma Jiji ni timu nzuri si timu mbaya inajikakamua vizuri kwahiyo hatuwezi kuwadharau ni timu nzuri, tumejiandaa kwa makusudi kupata alama tatu” 

Siwa ameyasema maneno punde tu baada ya kukanyaga ardhi ya Dodoma akiwa na msafara wa timu hiyo kwenye uwanja wa ndege jijini humo wakitokea jijini Dar es Salaam ambapo walikuwa na mchezo dhidi ya Ihefu na kushinda mabao 2-0 yote yakifungwa na Feisalum Salum Abdallah 'Fei toto'.

Yanga ipo nafasi ya pili ikiwa na alama 73, alama 7 nyuma ya bingwa Simba ilhali Dodoma Jiji ipo nafasi ya 9 ikiwa na alama 43 baada ya timu zote kukamilisha michezoya mzunguko wa 33 na kusaliwa na mchezo mmoja wa mzunguko wa 34 na kutamatisha ligi kuu siku ya kesho.

Ikumbukwe kuwa, kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza, Yanga iliinyuka Dodoma Jiji kwa mabao 3-1 mchezo uliochezwa kwenye dimba la Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.