Jumatano , 20th Aug , 2014

Msimu wa ligi kuu 2014-15 utaanza Septemba 20 huku ligi ya msimu huu ikiwa na mechi za mwisho wa juma pekee. Katikati ya juma kutatumika kwa mechi za viporo.

Ratiba ya Ligi Kuu msimu wa 2014-15

Ratiba ya Ligi Kuu Soka Tanzania Bara msimu wa 2014-15, imetoka mchana wa leo. Ratiba hiyo imezingatia michuano ya Chalenji itakayochezwa Novemba, usajili wa dirisha dogo Nov 15- Des 15, ushiriki wa klabu za Azam na Yanga kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa (CL) na Kombe la Shirikisho (CC).

Mechi zitachezwa wikiendi ili kuongeza msisimko na kuwapa fursa mashabiki wengi zaidi kuhudhuria, katikati ya wiki imeachwa wazi kwa ajili ya mechi za Kombe la FA (Federation Cup) ambapo mtendaji mkuu wa bodi ya ligi bwana Silas Mwakibinga amesema michuano hiyo itashirikisha timu za ligi kuu, timu za daraja la kwanza na mabingwa wa mikoa na itachezwa kwa mtindo wa mtoano.

Mara nyingi ratiba haizingatii umbali wa kijiografia. Mwa mfano, timu inapangiwa kucheza na Kagera Sugar mjini Bukoba, halafu inapangiwa kucheza na Coastal Union mjini Tanga na wiki inayofuatia wanapangiwa kucheza na Stand United mjini Shinyanga...wakati ingewezekana kucheza na Kagera halafu ikacheza na Stand United ili imalize mechi zote za kanda ya ziwa...lakini bwana Mwakibinga anasema mwaka huu ratiba imezingatia sana hilo lakini ni vigumu kuziridhisha timu zote

Ratiba hiyo inaonesha ligi itaanza Septemba 20 kwa mechi Tisa kuchezwa ambapo mabingwa watetezi Azam FC wataanza na Polisi Morogoro kwenye uwanja wa Azam Complex huku Yanga wakianza na Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Simba wataingia dimbani Septemba 21 kuwavaa binamu zao Coastal Union katika uwanja wa taifa jijini DSM.