Jumatano , 9th Sep , 2015

Kuelekea msimu mpya wa ligi kuu ya Soka Bara itakayoanza kutimua vumbi Jumamosi ya wiki hii, kikosi cha Tanzania prisons kimesema kipo katika maandalizi ya mwisho kwa ajili ya kuvaana na Azam FC na kuchukua pointi tatu muhimu.

Kocha msaidizi wa Tanzania Prisons Shaban Kazumba amesema, licha ya kutokuwa na wachezaji wa kimataifa katika kikosi hicho lakini Azam FC hawatawasumbua kwani mazoezi wanayoyapokea wachezaji kutoka kwa kocha mkuu Salum Mayanga yanatosha kabisa kuweza kufanya vizuri katika mechi hiyo na zilizo mbele yao.

Kwa upande mwingine Kazumba amesema, Shirikisho la Soka nchini TFF linatakiwa kuwa makini ili kuweza kudhibiti shutuma za rushwa kwa waamuzi zilizokuwa zikipelekea upangaji wa matokeo ili kufanya michuano hiyo kuchezwa kwa haki.

Kazumba amesema, kupunguza waamuzi haichangii kupunguza vitendo vya rushwa hivyo wanachotakiwa ni kuonyesha mfano kwa muamuzi atakayeendeleza vitendo hivyo kwa kutafuta wapelelezi makini watakaopambana na vitendo hivyo kwani wao kama makocha wanaumia wanapofundisha wachezaji na mwisho wa siku waamuzi wanashindwa kuchezesha mchezo wa haki na usawa.