Alhamisi , 3rd Jun , 2021

Mlinzi wa kulia wa timu ya taifa ya England, Trent Alexander-Anorld amepata maumivu ya nyama za paja kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Austria uliomalizika kwa England kupata ushindi wa bao 1-0 usiku wa kuamkia leo.

Anorld akiwa anatolewa nje ya uwanja dakika za lala salama baada ya kupata maumivu ya misuli kwenye mchezo wa usiku wa jana dhidi ya Austria, England ilishinda 1-0.

Anrold ambaye alitemwa kwenye kikosi hicho mwezi Machi mwaka huu kufuata kuporomoka kiwango, lakini siku mbili zilizopita alijumuishwa kwenye kikosi cha wachezaji 26 kitakacho shiriki michuano ya UEFA EUROS 2020 Juni 11 mwaka huu kwenye miji 12 mikubwa Ulaya.

Baada ya kujumishwa kwenye kikosi hicho, mjadala wa awali kwa wafuatiliaji wa soka Ulimwenguni walikuwa na kiroho juu kusubiri uteuzi wa kikosi hicho kujua nani atatemwa kati ya Kieran Trippier, Kylie Walker na Reece James.

Lakini haikuwa bahati kwa nyota huyo ambaye alikuwa anacheza mchezo wake wa kwanza tokea Machi kwa upande wa timu ya taifa kupata maumivu hayo ambayo yameibua hofu ya kutemwa kama yatamuweka nje kwa zaidi ya wiki mbili kwani EURO itaanza June 11, 2021.

Katika kuzungumzia hali ya maumivu ya mchezaji huyo, Kocha wa England, Gareth Southgate amesema, “Inabidi tusubiri tuone, imembidi atoke uwanjani sio ishara nzuri na alikuwa kwenye mazingira ambaye hayakuwa yanampa uhuru wa kutembea vizuri”.

“Ni mbaya kwa mchezaji yeyote kuumia kwasababu tupo karibu sana na mashindano kuanza, majeraha yatawapa wasiwasi. Lakini itabidi tusubiri ndani ya masaa 48 kujua ataendeleaje”.

Southgate alikwepa kutaja jina la mchezaji mwengine ambaye atamjumuisha kikosini endapo Anorld atalazimika kukaa nje kwa muda mrefu na badala yake akasema:

“Ngoja tuone, lakini Trent ndiye wa kwanza kwasasa”.

England itashuka tena dimbani siku ya Jumapili June 6, 2021 kukipiga na Romania kabla ya kucheza mchezo wake wa kwanza wa michuano ya EUROS 2020 na Croatia makamu bingwa wa Dunia.