Jumatatu , 30th Nov , 2015

Kiungo Jonas Mkude na Beki Shomari kapombe wameinyima The Kilimanjaro Stars nafasi ya kuelekea katika nusu fainali ya michuano ya Chalenji baada ya kukosa penati na Kill Stars kufungwa mikwaju ya Penati 4-3 na wenyeji Ethiopia.

Hatua ya penati ilifikiwa baada ya timu zote mbili kutoa sare ya bao 1-1 katika dakika 90 ya mchezo ambapo Tanzania ndio walioanza kujipatia bao lake la kwanza kupitia kwa John Bocco katika dakika ya 25 ya mchezo.

Kipindi cha kwanza cha mchezo kilikamilika huku Tanzania ikiwa mbele kwa bao 1-0 dhidi ya Ethiopia lakini katika kipindi cha pili cha mchezo Ethiopia ilijipatia bao lake la kusawazisha ndani ya dakika ya 57 kupitia kwa Gatoch Panom hivyo kupelekea timu zote kuwa sare ya bao 1-1 mpaka dakika 90 za mchezo.

Akizungumza baada ya mechi hiyo, kocha mkuu wa The Kilimanjaro Stars Abdallah Kibaden amewalalamikia waamuzi katika mchezo huo kuwa wamechangia wao kushindwa kusonga mbele katika michuano hiyo.