Wadau wa mchezo wa Mieleka ya ridhaa wakiuanda uwanja wa mchezo huo.
Hali ya ukata wa fedha kwa vyama vya michezo mbalimbali nchini Tanzania imeendelea kuathiri ushiriki wa timu za michezo mbalimbali katika medani ya kimataifa na hivyo taifa kupoteza nafasi ya kushiriki michuano hiyo mfano ukiwa michuano ya Olimpiki.
Baada ya hivi karibuni kushuhudia timu za taifa za michezo ya Ngumi na Judo zikishindwa kusafiri kwenda nje ya nchi kushiriki michuano ya kufuzu Olimpiki hali hiyo imeikumba pia timu ya mchezo wa mieleka ya ridhaa ambayo nayo ilikuwa iende nchini Algeria kushiriki michuano ya kufuzu kwa Olimpiki lakini ikakwama kutokana na ukata wa fedha na hivyo kuvunja kambi yao rasmi na kujiondoa kabisa katika michuano ya Olimpiki.
Akitangaza uamuzi huo katibu mkuu wa chama cha mieleka ya ridhaa nchini Tanzania AWATA Eliakim Melkizedeck amesema walijaribu kwa kila njia kutafuta udhamini wa safari ya timu hiyo kwa makampuni mbalimbali na hata serikali ili iweze kwenda nchini Algeria hawakufanikiwa na hivyo kushindwa kwenda na kuamua kuvunja kambi ya timu hiyo mpaka itakapotangazwa baadaye kwaajili ya ushiriki michuano mingine ya kimataifa.
Kutokana na hali hiyo Melkizedeck amesema wao AWATA na wanachama wengine wa umoja wa vyama vya michezo vilivyotarajiwa kushiriki michuano ya Olimpiki mwaka huu watakutana kujadili changamoto hizo za kukosa udhamini na pia kujipanga jinsi ya kusaidiana hasa vile vyama ambavyo vimefanikiwa kupata wawakilishi watakaokwenda kushiriki Olimpiki ya Rio nchini Brazil itakayoanza mapema mwezi wa nane mwaka huu.
Wakati huo huo Melkizedeck ameiomba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia baraza la michezo nchini BMT na wizara inayohusika na michezo kuwasaidia kukomboa uwanja wa mchezo wa mieleka ambao uko bandarini jijini Dar es Salaam.
Melkizedeck amesema uwanja huo wa kisasa wenye thamani ya kiasi cha shilingi milioni 450 za Tanzania umetolewa kama msaada toka nje hivyo kutokana na wao kukosa fedha za kulipia ushuru wanaiomba serikali iwasaidie kukomboa uwanja huo ambao kwa kiasi kikubwa utakuwa umesaidia kutatua moja ya changamoto kubwa za mchezo huo Tanzania bara na visiwani kwa ujumla.