Jumapili , 29th Dec , 2019

Aliyekuwa kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amejibu kuwa  anaidai Yanga fedha zake kwa nguvu kutokana na viongozi wa klabu hiyo kumuonesha dharau na kumundoa bila sababu ya msingi.

Makao Makuu ya klabu ya Yanga

Amesema amelazimika kulipa wanasheria kutoka Ulaya kusimamia suala hilo ikiwemo kulifikisha FIFA kutokana na dharau iliyooneshwa na viongozi wa Yanga, hasa Mwenyekiti Dkt. Mshindo Msolla ambaye mwanzo alimwambia kuwa kutokana na mambo anayoyafanya ndani ya Yanga hatoweza kuthubutu kumuondoa lakini baadaye alimgeuka.

"Huwezi kuwa kiongozi unayefanya mambo yako bila kujua kesho yatakuwaje, mimi ingelikuwa wameniondoa kutokana matokeo mabaya nisingefuatilia hela hii, ningekuwa nimefungwa mechi 4 mfululizo halafu wakaniondoa nisingedai chochote. Lakini kutokana na dharau nimeamua nidai", amesema Zahera.

"Simba wao wamemuondoa kocha wao na kesho yake wakamlipa pesa yake yote, Azam FC wamevunja mkataba na kocha wao kisha wakamlipa. Sasa hawa viongozi wananipigia simu kuwa mambo yako sawa, nakuja hapa hakuna yoyote anayenipigia kila mmoja anasema subiri tutakupigia" - Mwinyi Zahera

Aidha Zahera ameshindwa kutaja kiasi cha pesa anayoidai Yanga, huku akisema kuwa pesa anayoidai ni ya kawaida ambayo huwa anagawa kwa watu wasiojiweza kwao nchini Congo DR.

Ikumbukwe Zahera aliachana na uongozi wa klabu ya Yanga Novemba 05, 2019, ambapo Mwenyekiti wa klabu hiyo Dkt. Mshindo Msolla alisema waliamua kuanza upya.