Mechi ya leo kati ya Kagera na Mtibwa Sugar, katika dimba la Kaitaba Bukoba
Bao la Kwanza la Kagera limefungwa na Mbaraka Yusuph dakika ya 29, huku la pili likifungwa na Ibrahim Twaha dakika ya 53 na Mtibwa wamepata bao lake katika dakika ya 79 kupitia wa Stamil Mbonde.
Golikipa huyo wa Kagera Sugar alifariki usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya rufaa ya Bugando, hali iliyoufanya uongozi wa Kagera Sugar kuomba mechi hiyo kuahirishwa japo kwa siku moja, maombi ambayo hata hivyo yalikataliwa na TFF.
Sababu za TFF kugoma kuahirisha mchezo huo ni kutokana na maandalizi yaliyokuwa yamekwisha fanyika na kuwataka Kagera Sugar kujikaza kama Dida wa Yanga alivyojikaza kwa kucheza siku aliyofiwa na baba yake.
Wachezaji wa Kagera wakishangilia moja ya bao walilofunga
Kupitia mtandao wake wa Twitter, TFF iliandika "Dida wa Yanga alifiwa na baba mzazi alicheza mechi. Kanuni zingeahirisha mchezo kama ingekuwa siku ya mazishi."
Hata hivyo kutokana na kifo hicho, Rais wa TFF ametuma salamu za rambirambi kwa uongozi mzima wa Klabu ya Kagera Sugar inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara, familia ya marehemu, ndugu, jamaa, majirani na marafiki wa marehemu Burhan.
Marehemu David Burhan
Pia TFF limetangaza kuwa wachezaji wote watakaocheza mechi za leo na mwishoni mwa wiki wataomboleza kwa kuvaa vitambaa vyeusi mikononi.
Hatimaye mchezo huo umepigwa na kushuhudia Kagera Sugar wakinyakua pointi 3 na kujiongezea point kwenye msimamo wa ligi ambapo sasa imefikisha pointi 37 katika michezo 21 na kushika nafasi ya 3.
Katika mchezo mwingine uliopigwa leo, JKT Ruvu imetoka suluhu na Stand United katika mchezo uliopigwa dimba la Mkwakwani mkoani Tanga.