Alhamisi , 10th Dec , 2015

Klabu ya Kagera Sugar imewasili mkoani Tabora tayari kwa mtanange wake wa ligi kuu ya soka Tanzania bara dhidi ya Ndanda kutoka Mtwara utakaopigwa Jumamosi hii kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini humo.

Kikosi cha Kagera Sugar katika picha kabla ya kuikabili Yanga Oktoba 31, 2015

Akizungumza na East Africa Radio katibu mkuu wa wakata miwa hao Hamis Madaki amesema licha ya kujiandaa vyema lakini bado wanakosa hamasa ya mashabiki wao kutokana na marekebisho ya uwanja wao wa nyumbani wa Kaitaba kutokukamilika.

Hata hivyo Madaki amesema kuwa kutokana na mabadiliko ya benchi la ufundi la kumleta Adolph Rishard na kufanya usajili katika dirisha dogo la usajiri ana imani watajikwamua katika nafasi hii waliyo nayo na hatimaye kufanya vyema kwenye ligi kuu.

Kagera Sugar imekuwa na matokeo mabaya msimu huu ikiwa chini ya kocha Mbwana Makata ambaye tangu aanze kukifundisha kikosi alifanikiwa kupata ushindi kwenye mechi moja pekee, akipoteza saba na kutoa sare mchezo mmoja na mpaka sasa kikosi hicho kinashika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa timu 16 za ligi hiyo ikiwa na pointi tano tu.