John Bocco: Yanga hawatoki!

Jumatatu , 3rd Mei , 2021

Nahodha na mshambuliaji wa klabu ya Simba, John Rafael Bocco amejinasibu kuwa wataibuka na ushindi mbele ya watani wao wa jadi, klabu ya Yanga siku ya Jumamosi Mei 8, 2021 kwenye mchezo wa Ligi kuu bara utakaochezwa kwenye dimba la Mkapa jijini Dar es Salaam.

Mshambuliaji na Nahodha wa klabu ya Simba, John Rafael Bocco.

Bocco ameyasema hayo baaada ya Simba kutinga hatua ya robo fainali ya kombe la Shirikisho la Azam kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sukari jijini Dar es Salaam huku akiwashukuru mashabiki wa Simba kwa kuwa na moyo wa kuwaunga mkono.

Bocco amesema, “Kuelekea mchezo huo, tunaamini mchezo utakuwa mgumu, lakini ni kujipanga tu tunaamini timu yetu ina wachezaji wazuri, wachezaji wazoefu kwa hiyo tunaamini tutapambana na tutaweza kupata matokeo mazuri katika huo mchezo”.

Bocco ambaye ameshaifunga Yanga mabao 10 alipokuwa anaichezea klabu ya Azam, ameizungumzia hali ya watani wake wa jadi, Yanga kwa kusema;

“Kwanza tunawaheshimu wapinzani, ni timu nzuri ukiangalia hata mwanzo wa msimu walianza vizuri na hata ukiangalia wanavyocheza wanacheza vizuri, lakini tunaamini upande wetu tutajipanga vizuri na tunaweza kupata matokeo mazuri ya alama tatu kwenye mchezo huo”.

Mchezo huo unaotazamiwa kuwa wenye upinzani mkali kutokana na wawili hao kuwa kwenye mbio za ubingwa wa VPL, Simba akiwa ni kinara akiwa na alama 61, alama nne mbele ya Yanga anayeshika nafasi ya pili akiwa mbele ya Simba kwa michezo miwili, akiwa ana michezo 27.

Mchezo huo ni wa mzunguko wa pili wa VPL baada ya sare ya bao 1-1 kwenye mzunguko wa kwanza, pia unataraji kuwa mchezo wa 108 baada ya wawili hao kukutana mara 107 kwenye michuano yote, Yanga akishinda michezo 37, Simba michezo 32 na kutoka sare michezo 38.