Jumatano , 13th Jan , 2016

Kocha wa Mtibwa Sugar Meck Mexime amesema, katika mchezo wa Fainali utakaopigwa hii leo dhidi ya URA ya nchini Uganda hawataangalia kucheza vizuri au vibaya bali wanachoangalia wao mpaka mwisho wa mchezo ni kuchukua kombe.

Mexime amesema, URA sio timu mbovu na ndio maana goli lao ni gumu kulishambulia na wakifanya mashambulizi katika goli la wapinzani wanapata goli kwa haraka sana hivyo kwa upande wao hawataangalia pasi nyingi au kuingia golini bali wanatafuta ushindi katika mashindano hayo.

Mexime amesema, katika kundi lake alikuwa na wakati mgumu kwani ameshakutana na timu zote ngumu hivyo anaamini kikosi chake kitaweza kuibuka na ushindi.

Mexime amesema, kwa upande wa mikwaju ya penati hakuna mchezaji mbovu kwani kila mchezaji anaweza akakosa, lakini hawatarajii kufika katika hatua hiyo na wanawaomba mashabiki waweze kuwapa sapoti .

Kwa upande wake Nahodha wa Timu ya URA Simon Massa Masaba amesema, Mtibwa hawana tofauti kubwa sana na Simba, Yanga au Azam FC hivyo wanaamini watashinda kwani timu zote wanazijua.

Massa amesema, kila timu ilikuja kwa ajili ya kuchukua kombe hivyo wao wamezidi na wataweza kuchukua kombe kwani timu zote ni za Afrika Masharikina wanaujua mchezo wao.

Kwa upande wake Kiongozi wa Ulinzi wa URA Mwangizi Fredy amesema, wanaamini watachukua kombe kwani wanajiamini na wanabadilika katika kila mchezo hivyo kwa Mtibwa wanaamini watawafunga na kuweza kuibuka na ushindi.
Mtibwa iliingia katka hatua ya Fainali baada ya kuifunga Simba SC bao 1-0 huku URA ikiingia katika hatua ya Fainali baada ya kuitoa Yanga kwa mikwaju ya Penati 4-3.

Michuano hiyo iliyoanza kutimua vumbi Januari 04 ikishirikisha timu nane kutoka Tanzania Bara, Zanzibar na moja ya Uganda inahitimishwa leo hii kwa kupigwa mchezo wa Fainali utakaowakutanisha Mtbwa Sugar ya Tanzania Bara na URA ya nchini Uganda mchezo utakaopigwa Uwanja wa Amaan majira ya saa 20:15 usiku.