Jumatatu , 11th Jan , 2016

Raisi mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete amekutana na mshambuliaji wa Mbwana Samatta kumpa pongezi nyota wa kimataifa wa Tanzania Mbwana Samatta kwa ushujaa wa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa ndani Afrika.

Mbwana Samata akiwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete.

Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), amempongeza Samatta kwa mafanikio hayo huku akitoa siri ya mafanikio hayo kuwa ni kuzingatia wosia wake aliompa mjini Kinshasa, DR Congo wa kumtaka apambane na kuhakikisha anacheza soka barani Ulaya.

Katika mkutano na waadishi wa habari uliofanyika ofisi ndogo za CCM, Lumumba jijini Dar es salaam, Rais Kikwete alisema ana kila sababu ya kumpongeza straika huyo ambaye anaelekea Genk ya Ubelgiji kama mambo yote yataenda sawa.

Dkt. Kikwete amemtaja nyota huyo kuwa ndiye mkombozi wa taifa ambalo limekuwa na ukame kwenye michezo huku akiiomba wizara husika ya michezo kuhakikisha wanamsaidia katika kila hatua.

Kwa upande wa Samatta amempongeza JK na serikali ya awamu ya nne kwa kuwa naye bega kwa bega kwa kila hatua aliyoipiga.

Aidha, Samatta alimkabidhi Kikwete zawadi ya jezi ya TP Mazembe No 9 aliyokuwa akivaa klabuni hapo ambayo anaiacha baada ya kupata klabu mpya Ubelgiji anakoelekea sasa.