Kipa wa timu ya vijana ya chini ya miaka 20 ya Azam FC Hamad Juma akiwa amebebwa baada ya kuokoa penati dhidi ya Simba.
Timu ya vijana wenye umri chini miaka 20 ya Azam FC, imetinga nusu fainali ya mashindano ya Rolling Stone yanayoendelea jijini DSM, baada ya kuifunga timu ya vijana ya Simba kwa penati 3 kwa 2
Shujaa wa Azam FC alikuwa ni kipa wao, Hamad Juma aliyepangua penalti mbili za wachezaji wa Simba SC, Dadi Yunus na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’
Waliofunga penalti za Simba SC ni Ibrahim Hajibu na Omary Hussein wakati penalti za Azam zilifungwa na Kassim Kisengo, Reyna Mngungila na Adam Omar
Kipa wa timu ya taifa ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Peter Manyika alipangua penalti mbili pia za Shirazy Abdallah na Masoud Abdallah, lakini akaangushwa na wachezaji wake waliokosa penalti
Kipa wa Azam FC, Hamad Juma alichomoka kwa shangwe baada ya kupangua mkwaju wa mwisho wa Tshabalala aliyesajiliwa kwa ajili ya kikosi cha kwanza cha Simba SC kutoka Kagera Sugar msimu huu
Peter Manyika aliyefanya kazi nzuri ya kuokoa michomo mingi ya hatari ndani ya dakika 90 na akaenda kucheza penalti mbili baadaye aliangua kilio baada ya mchezo huo kutokana na kutoamini matokeo hayo
Na mara baada ya mchezo kocha mkuu wa timu ya vijana ya Simba Nicko Kiondo amesema amepokea matokeo hayo kama changamoto na kwa sasa anajipanga upya kwa michuano ijayo
Naye Idd Nassoro Cheche kocha msaidizi wa timu ya vijana ya Azam FC ambayo imetinga nusu fainali ya michuano hiyo amesema walistahili ushindi katika mchezo huo kwakuwa wanamaandalizi ya muda mrefu takribani mwaka mzima wakijiandaa na ushindi huo wameupokea kwa mikono miwili
Kwa ujumla mchezo ulikuwa mzuri na timu zote zilishambuliana kwa zamu, huku wachezaji wakionesha vipaji vya hali ya juu. Kwa kutolewa, Simba SC imeungana na watani wao, Yanga SC ambao jana walitolewa katika hatua ya 16 Bora.
Nusu Fainali zinatarajiwa kuchezwa kesho