Jumamosi , 17th Jul , 2021

Washika mitutu wa jiji la London, klabu ya Arsenal imefikia makubaliano kumsajili mlinzi wa kati, Ben White wa klabu ya Brighton & Hove Albion kwa ada ya uhamisho wa paundi milioni hamsini za England ambazo ni sawa na bilioni mia hamsini na tisa na zaidi ya milioni mia sita za kitanzania.

Ben White alipokuwa anaitumikia Brigthon & Hove Albion kwenye moja ya mchezo wa EPL msimu uliopita.

Makubaliano ya usajili wa nyota huyo mwenye umri wa miaka 23 raia wa England ni kusaini kandarasi ya miaka mitano ambayo itamfanya awatumikie washika mitutu hao kuanzia Julai mwaka huu hadi juni 30 mwaka 2026.

Ben White amewindwa na Arsenal baada ya kuonesha kiwango kizuri msimu uliopita kwa kucheza nafasi ya mlinzi wa kati na mara kadhaa mlinzi wa kulia ma kuisaidia Brighton kwenye mapambano ya  kutoshuka daraja na kushika nafasi ya 16.

Mbali na kusalia EPL, lakini Brighton imekuwa pekee kuruhusu mabao machache, mabao 46 kwenye orodha ya timu kuanzia nafasi ya kumi hadi kwa Sheffield United iliyoshika mkia na kushuka daraja jambo lililopelekea kumfanya ajumuishwe kwenye kikosi cha wachezaji 23 walioshiriki UEFA EUROS licha ya kutocheza mchezo hata mmoja.

Arsenal wamelazimika kusaka mlinzi wa kulia baada ya mlinzi wao wa sasa, Hector Bellerin kuiambia klabu hiyo kuwa anataka kutimkia Inter Milan ya Italia ili kuenedelea kusaka changamoto mpya kwenye maisha yake ya soka.

Arsenal pia itakamilisha usajili wa kiungo Albert Sambi Lokonga kutoka Anderletch ya Ubelgiji pindi nyota huyo atakapomaliza siku za kukaa karantini hivi karibuni kwa gharama za paundi milioni kumi na tano ambazo ni sawa na bilioni arobaini na saba na zaidi ya milioni mia tisa za kitanzania.