
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo, Yusuph Singo
Waziri Mwakyembe aliuleta mjadala huo wakati akisoma mapendekezo ya bajeti ya Wizara yake bungeni, Aprili 22, ambapo pamoja na mambo mengine alisisitiza kuwepo na haja ya majadiliano ya Kitaifa juu ya kuangalia idadi ya wachezaji wa kigeni wanaotakiwa nchini ili kuwapa nafasi zaidi wachezaji wazawa.
Akizungumzia mjadala huo kwa upande wa wizara, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo wa wizara, Yusuph Singo amesema kuwa Waziri Mwakyembe hakutoa hitimisho la mjadala huo wala hakuelekeza ni idadi gani inahitajika, bali alitoa maelekezo kwa BMT kusimamia mjadala kwa kukusanya maoni ya Watanzania na wadau wa michezo.
"Waziri Mwakyembe ameiagiza BMT kukusanya maoni ili kuona njia gani nzuri ambayo itakuja nayo, kwa sababu nchi haiwezi tu kuachia soko huria bila ya mipaka", amesema Singo.
"Miongozo ambayo tutakuja nayo baada ya kupata maoni itakuwa na faida nyingi, siyo tu kudhibiti wachezaji, lakini pia kuweka ulinzi wa mikataba yao kwa sababu kuna wachezaji wamejikuta wanasaini mikataba miwili miwili", ameongeza.