Waziri aagiza madeni yalipwe kabla ya Disemba

Thursday , 12th Oct , 2017

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Said Jafo, amesema halmashauri 12 nchini zimekuwa wadaiwa sugu wa fedha wanazokopa katika bodi ya mikopo ya serikali za mitaa, hivyo kutakiwa kulipa kabla ya Desemba 30.

Amesema halmashauri hizo zinadaiwa zaidi ya shilingi bilioni mbili  huku halmashauri ya wilaya ya mbinga ikiongoza kwa kudaiwa kiasi kikubwa, hivyo kumuagiza mtendaji mkuu wa bodi hiyo, Richard Mfugale, kufuatilia wadaiwa hao ili waweze kurejesha mikopo yao kabla ya Desemba 30, mwaka huu.

Mtendaji Mkuu wa bodi hiyo, Richard Mfugale, amesema halmashauri ya Mbinga ndiyo ina mzigo mkubwa wa deni pamoja na halmashauri ya Jiji la Mbeya fedha walizokopa zikiwa kwa ajili ya kujenga vitega uchumi kama ukumbi na bweni za Mkapa lakini ulipaji umekuwa wa kusumbua na deni kufikia shilingi milioni 914.

Halmashauri zinazodaiwa na bodi hiyo ni Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Mbeya, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Singida, Morogoro, Halmashauri ya wilaya Kigoma, Karatu, Pangani, Igunga, Kongwa na Halmashauri ya Mbinga na Mji Mbinga.