Utafutaji huu mpya, ambao utaendelea kwa siku 55, ulianza Machi lakini ukasitishwa muda mfupi baadaye kwa sababu ya hali mbaya ya hewa.
Ndege ya MH370, Boeing 777, ilitoweka mwaka 2014 ilipokuwa ikisafiri kutoka Kuala Lumpur kuelekea Beijing na kusababisha msako mkubwa zaidi katika historia ya usafiri wa anga.
Kampuni ya utafutaji Ocean Infinity inaongoza utafutaji wa sasa chini ya mkataba wa "usipoipata, hulipwi.” Itapokea dola milioni 70 (£56m) ikiwa mabaki hayo yatapatikana, Waziri wa Uchukuzi Loke Siew Fook alisema.
Majaribio ya awali ni pamoja na utafutaji uliohusisha meli 60 na ndege 50 kutoka nchi 26, ambao ulimalizika mwaka 2017, na jitihada za 2018 za Ocean Infinity zilimalizika baada ya miezi mitatu.
Ndege ya MH370 ilipoteza mawasiliano chini ya saa moja baada ya kupaa tarehe 8 Machi 2014, na rada ilionyesha kuwa ilikuwa imetoka kwenye njia yake ya awali ya ndege.
Katika uchunguzi wa mwaka 2018, wachunguzi walisema "majibu kamili yatapatikana ikiwa mabaki yatapatikana."


