Jumatano , 3rd Dec , 2025

Mfanyabiashara Jennifer Jovin (26) maarufu kama Niffer na Mika Chavala, ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi ya uhaini katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wameachiwa huru leo Desemba 3, 2025.

 

Wawili hao walikuwa sehemu ya washitakiwa 22 kwenye kesi namba 26388/2025, ambapo 20 kati yao walifutiwa mashtaka Novemba 25, 2025.

Uamuzi huo umetolewa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, baada ya Wakili wa Serikali Titus Aron kueleza kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hana tena nia ya kuendelea na kesi dhidi yao, kwa mujibu wa Kifungu cha 92(1) cha Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA).

Baada ya maelezo hayo, Wakili wa utetezi, Peter Kibala, alisema hawana pingamizi, na aliomba mahakama itoe tamko rasmi la kuwaachia huru wateja wake.

Hakimu Lyamuya alikubali ombi hilo na kutamka kwamba washitakiwa wameachiliwa huru, isipokuwa kama wanashikiliwa kwa shauri jingine.