Jumatano , 3rd Dec , 2025

Kocha wa Liverpool, Arne Slot, amefichua kuwa Mohamed Salah hakuwa na furaha baada ya kuachwa nje ya kikosi cha kwanza kilichocheza dhidi ya West Ham United katika mchezo wa EPL uliomalizika kwa ushindi wa 2-0 kwa Liverpool.

 

Salah (33) alianza benchi katika mechi hiyo iliyopigwa jijini London, ikiwa ni mara ya kwanza kutokaanza mechi tangu Slot achukue mikoba ya ukocha Anfield. Alexander Isak na Cody Gakpo waliongoza safu ya ushambuliaji kwenye ushindi huo.

"Ni wazi hakufurahi, na hilo ni jambo la kawaida kwa mchezaji wa kiwango chake," alisema Slot katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea mechi ya kesho dhidi ya Sunderland.  
"Salah amekuwa mchezaji muhimu kwa miaka mingi na ataendelea kuwa hivyo. Hivyo ni sahihi kusema hakuwa na furaha."

Kwa sasa, haijathibitika iwapo Salah atarejea kikosi cha kwanza kesho Jumatano dhidi ya Sunderland, au kama Slot ataendeleza mfumo uliomletea ushindi dhidi ya West Ham.

Kiwango cha Salah kimeonekana kushuka kidogo hivi karibuni, huku Liverpool ikipata matokeo duni kwenye mechi tisa kati ya 12 zilizopita kabla ya ushindi huo.