Jumanne , 8th Jul , 2014

Jeshi la Polisi nchini Tanzania linawashikilia watu wawili, kuhusiana na mlipuko uliotokea katika mgahawa karibu na viwanja vya Gymkhana na Mahakama Kuu Jijini Arusha jana usiku ambapo watu wanane wamejeruhiwa vibaya huku mmoja akiwa mahututi.

Mkurugenzi wa makosa ya jinai nchini Tanzania DCI Issaya Mngulu.

Mkurugenzi wa Makosa ya jinai nchini Tanzania kamishna wa polisi DCI Issaya Mngulu, ametoa taarifa hiyo katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar-es-Salaam leo, huku akiwataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kuepuka mikusanyiko isiyo na lazima.

Kwa mujibu wa kamishna Mngulu, matukio ya milipuko inayoendelea kutokea sehemu mbali mbali nchini hivi sasa ni sehemu ya kukua kwa mtandao wa uhalifu wa kimataifa, na kuongeza kuwa jeshi hilo linawatilia shaka zaidi ya watu ishirini na tano ambao inadhani wanastahili kuchunguzwa na kuhojiwa kuhusiana na matukio hayo ya milipuko.

Aidha DCI Mngulu amewataka wanaoitisha mikusanyiko kuhakikisha wanachukua tahadhari ya kutosha kuepusha kutokea kwa matukio hayo ikiwa ni pamoja na kutumia vifaa vya kisasa vya kuzuia na kunasa matukio ya uhalifu.