Jumatano , 25th Mar , 2015

Zaidi ya watu 90 hugundulika kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu kila baada ya miezi mitatu katika manispaa ya Iringa.

Moja ya bango linalotoa ujumbe kuhusu Kifua Kikuu.

Mratibu wa Kifua kikuu na Ukoma mkoa wa Iringa Dk. Tekla Urio amesema kila mmoja anaweza kuwa na vimelea vya ugonjwa kifua ingawa bado kinga za mwili hazijashuka ili ugonjwa huo kujionyesha.

Dr Urio amesema hayo leo katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa katika Maadhimisho ya kifua kikuu Duniani ambapo amesema wametumia siku hii kuelimisha jamii pamoja na kuwahimiza wananchi kujitokeza kupima ugonjwa wa kifua kikuu.

Aidha Dk. Urio amesema ugonjwa wa kifua kikuu unaambukizwa kwa njia ya hewa na kwamba maeneo ya mikusanyiko ya watu yanayoweza kusababisha maambukizi ya kifua kikuu kutokana na kukosekana kwa hewa ya kutosha.

Ameongeza kuwa ikiwa mtu atapima mapema ugonjwa huo na kugundulika kuwa ameathiriwa anaweza kutibiwa na kupona kabisa.

Hata hivyo amesema halmashauri ya mufindi inaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wa kifua kikuu kutokana na wilaya hiyo kuwa na takwimu kubwa ya wagonjwa wa UKIMWI ikifuatiwa na Iringa vijijini, na Kilolo na kauli mbiu ya maadhimisho ya kifua kikuu mwaka huu ni IBUA, TIBU, PONYA KILA MGONJWA KIFUA KIKUU(TB).