
Picha ikionesha abiria ndani ya daladala ambao hawajachukua tahadhari juu ya ugonjwa wa Covid-19.
kuhakikishe magari ya usafiri wa umma wanapakia abiria kulingana na idadi ya viti pasipo kusimama.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi aliyasema hayo wakati akisoma mwongozo wa udhibiti wa ugonjwa wa korona (uviko-19) kupitia afua ya kuthibiti misongamano katika jamii bila kuathiri shughuli za kiuchumi toleo la kwanza.
Uchunguzi uliofanywa na mtandao huu katika baadhi ya maeneo ilikuta muitikio wa watu katika kuchukua tahadhari bado ni mdogo, wanaovaa barakao ni wachache ukilinganisha na idadi halisi ya watu waliopo katika maeneo hayo.
Jijini Dar es Salaam, daladala zimeonekana kuendelea kupakia abiria mpaka mlangoni na msongamano uliopo bado abiria hawajavaa barakoa na hakuna sanitaiza katika mabasi.
Maeneo ya masoko bado kumeonekana kuwepo kwa msongamano mkubwa wa watu na maeneo ya stendi hakujaonekana kuwa na miundombinu rafiki ya kujikinga kama maji tiririka na sabuni.
Maeneo kama soko la Shekilango, Sinza na hata Stendi ya Makumbusho watu wameonekana wakiendelea na shughuli zao kama kawaida bila kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi hivyo jambo ambalo linahatarisha maisha yao.
Lakini hali hiyo imeonekana si tu kwa mtu mmoja mmoja bali hata wamiliki wa biashara bado hawajawa na ule mwamko wa kuweka maji tiririka na sabuni kwa ajili ya wateja wanaowahudumia ikiwa ni moja ya njia ya kujikinga na virusi hivyo.
“Unaweza kuwa na maji lakini mtu hanawi, tulichofanya sisi tumeweka vitakasa mikono mlangoni na mtu haruhusiwi kuingia bila kutumia. Wapo wanaojifanya kuwa na haraka wakati mwingine kama mteja akishakuwa tayari yuko ndani ya duka inakyuwa ni ngumu kumrudisha nje,” alisema Joyce Mushi mfanyabiashara eneo la Kunduchi.
Jijini Tanga, maelekezo ya Serikali kuhusu kujikinga na korona yameanza kutekelezwa katika baadhi ya makampuni ya mabasi yaendayo mikoani hapa huku daladala zikiendelea kujaza abiria kana kwamba hakuna tishio lolote.
Mwandishi alipita katika ofisi ya kukatia tiketi ya kampuni ya mabasi ya Tashriff iliyopo barabara ya 14 jijini Tanga na kukuta mfanyakazi wake aliyejitambulisha kwa jina moja la Awadh akiwatangazia abira kwa kutumia kipaza sauti kuhusu kila mmoja kuvaa barakoa na kuwa na kitakasa mikono.
“Abiria wetu tunawaomba kabla ya kuingia kwenye mabasi hakikisheni mmevaa barakoa na kila anayeingia atapakwa kitakasa mikono…hali ni mbaya tunafanya hivi si kwa nia ya kuwasumbua bali kunusuru maisha yenu,” alisema Awadhi.
Katika kituo cha kikuu cha mabasi cha Kange Jijini Tanga ilishuhudiwa abiria katika baadhi ya mabasi yaendayo mikoani baadhi yao wakiwa wamevaa barakoa lakini wengine hawajavaa.
Kwenye daladala zimeendelea kuwasimamisha abiri ambapo walipozungumza na Mwananchi baadhi ya makondakta walisema utekelezaji wa abiria wanaokaa kwenye viti pekee utakuwa mgumu kwao.
Afisa wa mamlaka ya usimamizi wa usafiri wan chi kavu (Latra)mkoa wa Tanga,Kenedy Jakabondo alisema maafisa watapita katika vituo vyote vya mabasi kutangaza kuhusu mwongozo wa kujikinga na korona kwa kutumia gari.
Wakati Jijini Arusha Chama Cha wasafirishaji Mkoa wa Arusha na Kilimanjaro ( AKIBOA) kimeagiza madereva wa magari yote ya abiria kuhakikisha wanavaa barakoa na vitakasa mikono( sanitizer) ili kupambana na ugonjwa wa Corona ikiwa ni utekezaji wa Maagizo ya Serikali.
Katibu wa AKIBOA, Locken Adolf Masawe alisema madereva wote na wasaidizi wao wanapaswa kuvaa barakoa na kila gari kuwa na sanitizer.
"Tumeagiza pia kwenye vituo vya mabasi kuwa na maji tiririka ambayo abiria watanawa kabla ya kupanda kwenye magari," alisema.
Mkoa wa Arusha na Kilimanjaro ni miongoni mwa mikoa inayotajwa kuwa na maambukizi makubwa ya ugonjwa wa corona awamu ya tatu.
Moshi wakati Mamlaka ya Usafiri Ardhini (Latra) ikianza kudhibiti abiria wasiovaa barakoa katika kituo kikuu cha mabasi mjini Moshi, hali ni tofauti kabisa katika masoko ambapo wafanyabiashara na wateja wameonekana kuingia bila kujikinga.
Jana na juzi, Kaimu Afisa wa Latra mkoa Kilimanjaro, Joseph Umoti kwa kushirikiana na wasafirishaji na Jeshi la polisi walikuwa wakizuia mabasi kutoka katika kituo kikuu cha mabasi mjini Moshi kama kuna abiria hajavaa barakoa.
“Jana (juzi) tulikuwa kwenye mageti yote ya kutoka stendi kuhakikisha hakuna basi linatoka kama wahudumu na abiria hawajavaa barakoa. Leo (jana) niko hapa stendi mimi mwenyewe kuhakikisha tahadhari za corona zinachukuliwa,” alisema.
Mwenyekiti wa wasafirishaji mikoa ya Kilimanjaro na Arusha (Akiboa), Hussein Mrindoko alikiri Latra, Akiboa na Polisi kushirikiana lakini akataka elimu kabambe itolewe kwa abiria kwa sababu kuna mizaha mingi kwa baadhi ya abiria.
Wakati hali ikiwa hivyo katika kituo kikuu cha mabasi mjini Moshi, hali ni tofauti kwenye usafiri wa umma kama daladala na pia Bajaji na bodaboda ambako utaratibu wa kuvaa barakoa au kuwa na sanitizer umekuwa msamiati mgumu.