Ijumaa , 25th Sep , 2015

Watanzania wanne wamethibitishwa kufariki dunia katika tukio la kukanyagana katika mji wa Makka, ikiwa ni miongoni mwa mahujaji zaidi ya 700 waliopoteza maisha katika tukio hilo wakati wa siku ya mwisho ya Hijja.

Baadhi ya waokoaji na baadhi ya mahujaji wakiwa wanatoa miili na majeruhiwa tukio la kukanyagana kulipolekea vifo vya watu 717

Taarifa ya Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Abubakari Zuberi iliyotolewa akiwa Mekka imewataja watanzania watatu waliokwisha tambulika majina yao kuwa ni Bi. Mwanaisha Hassan Juma, Mkungwe Suleiman Hemedi na Sefu Saidi Kitimla.

Mtanzania mwingine mwanamke aliyekufa jina lake bado halijatambulika, pia yupo raia mmoja wa Kenya Bi. Fatuma Mohammed Jama ambaye alisafiri Mekka kwa kutumia wakala wa Tanzania.

Aidha ameongeza "Kuna taarifa ya mahujaji wanawake wawili ambao hadi Alhamisi usiku walikuwa hawajapatikana hivyo hakukuwa na uhakika juu ya usalama wao hadi tutakapowaona ama kupata taarifa zao."

Mufti Zuberi amesema pia kuwa taarifa za majeruhi miongoni mwa mahujaji wa Tanzania na baadhi ya majeruhi hao ambao wameweza kupatiwa matibabu na kuruhusiwa kutoka hospitalini.

Pia ameongeza kuwa ameagiza maafisa wetu wa Bakwata waliopo katika mji wa Mina kuendelea kufuatilia habari na taarifa za mahujaji katika hospitali na sehemu za kuhifadhia maiti.