Alhamisi , 25th Jun , 2015

Mkuu wa kituo cha Polisi Wilaya ya Chamwino, OCD Atubone Mwakalukwa ametoa siku kumi kwa wananchi wa kijiji cha Ilangali kilichopo kata ya Manda Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma kuzisalimisha silaha wanazomiliki kinyume cha sheria kabla msako mkali.

Baadhi ya silaha zilizowahi kukamatwa katika matukio ya Ujangili.

Mwakalukwa ametoa kauli hiyo leo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na umuhimu wa wananchi hao kushirikiana na wahifadhi wa misitu na mbuga za wanayapori zinazowazunguka katika kuweka ulinzi na kukabiliana na majangili.

Amesema baada ya siku hizo kupita jeshi la polisi litashirikiana na wahifadhi wa hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwa upande wa Dodoma na Iringa ili kufanya msako wa watu wanaomiliki silaha kinyume na sheria na kujihusisha na vietendo vya ujangili katika hifadhi hiyo.

Amesema yeyote atakayepatikana na hatia ya kumiliki silaha kinyume na sheria ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria za nchi na siyo sheria za uhifadhi wa wanyapori.

Amesema kuwa jeshi la polisi limepata taarifa kuwa kuna baadhi ya watu ambao wanamiliki silaha kinyume cha sheria na kuzikodisha kwa watu wanaofanya vitendo vya ujangili kwenye hifadhi za taifa na hivyo kutoa siku kumi kwa watu hao kuzisalimisha silaha hizo kwenye vituo vya polisi.

Amesema kuwa baada ya siku hizo kupita jeshi la polisi kwa kushirikina na vikosi vya uhifadhi ya Taifa ya Ruaha watafanya msako na atakayepatikana na silaha anayoimiliki kinyume cha sheria akipatikana na hatia mahakamani adhabu yake ni kifungo cha miaka 15 gerezani.

Kwa upande wake Mkuu wa Kanda kikosi cha kupambana na ujangili kutoka Mkoa wa Iringa, Majid Lalu amesema kuwa adhabu ya mtu atakayepatikana mahakamani na kosa la kuingia na silaha ndani ya hifadhi kinyume cha sheria ni kifungo cha mwaka mmoja hadi mitano au kulipa faini y ash. Laki mbili au vyote viwili kwa pamoja.

Amewatahadharisha wananchi hao kutofanya shughuli zote zilizokatazwa kufanywa ndani ya hifadhi za taifa ikiwemo kuchunga mifugo, kulima au kuwinda bila kibali.