Jumanne , 21st Mar , 2023

Baadhi ya wakazi wa vijiji vitatu kati ya vitano vilivyoko katika kata Karabagaine katika wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, wameondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kwenda kuchota maji kwenye vyanzo vya asili, na kuepuka ugomvi uliotokana na kugombania maji,

Hii ni baada ya mradi wa maji kuanza kutoa huduma katika vijiji hivyo

Wakizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji katika kata hiyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya maji, wakazi hao ambao ni kutoka katika vijiji vya Kitwe, Itahwa na Kiziru wamesema kuwa walipata matumaini baada ya serikali kuanza utekelezaji wa mradi huo

"Maji haya yametukomboa, tulipata shida sana hasa akina mama na pia  watoto ambao walitoka shule badala ya kupata muda wa kujisomea walipoteza muda mwingi kufuata maji mtoni, lakini pia tulikuwa tunafikia hatua ya kugombana yaani tunapigana kwa sababu ya maji hasa wakati wa msimu wa kiangazi" wamesema wananchi

Mhandisi Gadama Kulwa ni msimamizi wa mradi wa maji Karabagaine ambao unatekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba - BUWASA - akitoa taarifa ya mradi huo amesema kuwa hadi kukamilika kwake utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.8

"Mradi huu utahudumia vijiji vitano wa Kata ya Karabagaine ambavyo ni Kitwe, Itahwa, Kiziru, Kangabusharo na Ibaraizibu, vyenye wakazi 16,104" amesema mhandisi Kulwa

"Hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu, jumla ya vijiji 560 kati ya vijiji 660 vinavyosimamiwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini -RUWASA- vinapata huduma ya majisafi na salama, ambapo zaidi ya wakazi milioni 2.1 wananufaika" amesema mhandisi Gerome