Ijumaa , 25th Sep , 2015

Wakulima wadogo nchini wameendelea kulia na ushuru mkubwa wa mazao uliowekwa na serikali, ucheleweshwaji wa pembejeo na kushindwa kudhibitiwa kwa madalali wanyonyaji sokoni na kutaka serikali ijayo kuangalia upya masuala hayo.

Charles Meshack Mkurugenzi wa Shirika la kuhifadhi misitu ya asili Tanzania(TFCG).

Ushauri huo umetolewa na wakulima wadogo wakati wa mkutano wa wadau ulioshirikisha pia taasisi mbalimbali zinazo fanya kazi katika sekta ya kilimo na mabadiliko ya tabia nchi ambapo walishauri kubadilishwa kwa mfumo wa ushuru na kufikishiwa mapema pembejeo za kilimo pamoja na kupimiwa viwanja kwenye maeneo yao.

Wadau hao wa kilimo na mazingira waliishauri serikali ijayo kuyapa kipaumbele masuala ya maendeleo ya mazingira ikiwemo kuongeza bajeti ya kilimo, kutengwa sera mahususi ya mabadiliko ya tabia nchi, kutoa fedha kwa asasi zisizo za kiserikali ili kushirikiana kuendeleza maendeleo vijijini.

Mkutano huo ulioandaliwa na mtandao wa jamii unaohusika na usimamizi wa misitu ya asili Tanzania MJUMITAa, uliwahusisha wakulima wadogo na wawakilishi kutoka mashirika ya TFCG, Toam, MVIWATA, ANSAF, Forum CC, Care International, Policy Forum, Wopata, Taha na Briten.