Jumapili , 4th Sep , 2022

Mamlaka ya Maji safi na mazingira Wilaya ya Liwale, Mkoani Lindi (LIWASA) imeombwa kuzalisha kwa wingi huduma ya maji kwa lengo la kuwatatulia wananchi kero za upatikanaji wa huduma hiyo kwa jamii.

Uhaba wa maji Liwale

Ombi hilo limetolewa na baadhi ya wakazi wa mji wa Liwale walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa East Africa TV alipotembelea wilaya hiyo na kudai kukabiliwa na tatizo hilo kwa muda mrefu na kwamba wanalazimika kutumia maji yaliyotuwama kwenye mito.

Zaidi ya mwezi sasa hatupati huduma hii ya maji safi na salama kwa matumizi ya binaadamu” Walieleza wakazi hao.

Wakazi hao wameongeza kuwa kwa sasa hulazimika kununua dumu moja lenye ujazo wa Lita 20 kwa bei ya Sh. 1,000 hadi Sh. 1,500. Wameiomba Mamlaka ya Maji safi, salama na mazingira Liwale (LIWASA) kuzalisha rasilimali hiyo kwa wingi ili wananchi waweze kunufaika na huduma hiyo mhimu.

Changamoto ya upatikanaji wa maji ndani ya mji wetu ipo tena ni kubwa, kwani tunakaa wiki mbili hadi nne bila kupata maji, badala yake tunakunywa yaliyotuama mitoni”Alieleza Ridhiwani, Mkazi wa wilaya hiyo.