Ijumaa , 14th Feb , 2025

Serikali imesema kwamba taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba kampuni moja kutoka Saudi Arabia imepata mkataba wa uwekezaji wa kujenga na kuendesha Bandari ya Bagamoyo sio za kweli. 

Waziri wa Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo,

Taarifa hiyo imetolewa leo Februari 14, 2025 na Waziri wa Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo,  na kusema kuwa serikali ipo katika hatua mbalimbali za kutekeleza programu ya ujenzi wa eneo maalum la kiuchumi la Bagamoyo (Bagamoyo Special Economic Zone BSEZ), ikiwa ni moja ya miradi 17 ya kielelezo iliyopo katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22 - 2025/26. 

"Utekelezaji wa programu hii utafanywa na sekta binafsi kwa kushirikiana na serikali kupitia mpango wa ubia kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma (Public-Private Partneship-PPP), wakati wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wameonesha nia ya kuwekeza katika ujenzi wa miradi mbalimbali iliyopo katika programu ya BSEZ, na wapo katika hatua mbalimbali za mazungumzo na taasisi mbalimbali husika za serikali, serikali haijaingia makubaliano (commitment) yoyote na mwekezaji yeyote kwa sasa kutokana umuhimu na ukubwa wa programu ya BSEZ, umma utajulishwa kikamilifu katika kila hatua ya utekelezaji wake," imeeleza taarifa ya Profesa Kitila