Ijumaa , 14th Feb , 2025

Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limemkamata Emmanuel Mapana (24) maarufu kwa jina la Mchambi, mkazi wa mtaa wa Sima, wilaya ya Bariadi, akiwa na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania zenye cheo cha Luteni.

Luteni feki wa JWTZ

Tukio hilo limetokea leo Februari 14, 2025 majira ya saa 6:30 mchana, ambapo kikosi kazi cha kupambana na uhalifu mkoani Simiyu kilimkamata Emmanuel akiwa amevalia kombati za JWTZ na akiwa na gari aina ya Ractic lenye namba za usajili T.560 DCS. Baada ya upekuzi, alikutwa na mkanda wa JWTZ na kompyuta mpakato (laptop) moja.

Taarifa za awali zinaeleza kuwa Emmanuel amekuwa akijifanya mtumishi wa serikali kwa muda mrefu na alikuwa akitafutwa kwa tuhuma hizo.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuhakikisha usalama na utulivu vinaendelea kudumishwa.