Jumanne , 28th Apr , 2015

Wakazi wa mkoa wa Iringa wametakiwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura linalotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Mbunge wa iringa mjini Chadema Mchungaji Peter Msigwa akiongea katika moja ya mikutano ya Chama cha demokrasia na Maendeleo.

Mbunge wa Jimbo la Iringa mjini mh. Peter Msigwa amewataka wananchi kujitokeza na kuacha kuhofia foleni kwani kwa kuacha kujiandikisha watakuwa wamejikosesha haki yao ya msingi.

Aidha Mh. Msigwa ameongeza kuwa wamepanga kuhakikisha wanatatua changamoto ambazo zimeweza kujitokeza katika mkoa wa Njombe ili zisijirudie katika mkoa wa Iringa na kufanikisha zoezi hilo kwa ufanisi.

Katika hatua nyingine mbunge huyo amebainisha kuwa wamepanga mikakati ya kuwafanya wananchi wa mkoa huu kuendelea kupata elimu ya umuhimu wa kujiandikisha katika daftari hilo la wapiga kura kwa kuandaa mikutano katika maeneo yao.