Jumatatu , 14th Apr , 2014

Wizara ya ujenzi nchini Tanzania imesema kuharibika kwa miundombinu kulikotokana na mvua zilizonyesha kwa siku kadhaa maeneo mbali mbali nchini hakutokani na ubovu au uzembe wa wakandarasi waliojenga miundombinu hiyo.

Moja ya madaraja yaliyoharibiwa na mvua zilizonyesha sehemu mbali mbali nchini mwishoni mwa wiki

Waziri wa wizara hiyo Dkt John Pombe Magufuli, ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam, ambapo amezitaja barabara zilizoharibiwa na mvua kuwa ni ile ya inayounganisha mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro, barabara ya Bagamoyo, barabara inayounganisha jiji la Dar es Salaam na mikoa ya Lindi na Mtwara katika daraja la Kongowe pamoja daraja linalounganisha Kongowe na Mjimwema.

Kwa mujibu wa waziri Magufuli, serikali hivi sasa inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa mawasiliano kupitia barabara hizo yanarejea mara moja, ambapo amewataka mameneja wa wakala wa barabara (Tanroads) kwenye mikoa yote nchini kusitisha likizo zao za Pasaka ili wapate muda wa kusimamia ukarabati wa miundombinu hiyo.