Ijumaa , 19th Sep , 2014

Jukwaa la wahariri nchini Tanzania limesema litamwandikia barua mkuu wa jeshi la polisi IGP Ernest Mangu kutaka askari wote walioshiriki kuwapiga hadi kuwajeruhi waandishi wa habari hapo jana kuchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini Tanzania Absalom Kibanda (anayezungumza na simu) akisalimiana na Mhariri wa gazeti la Tanzania Daima Ansbert Ngurumo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo, Mwenyekiti wa Jukwaa hilo Absalom Kibanda amesema haamini kama askari waliowapiga waandishi wa habari wana taaluma na sifa za kuwa askari katika jeshi hilo.

Kwa upande wake Katibu wa Jukwaa la wahariri nchini Bw. Neville Meena amesema jukwa hilo halitaweza kuzuia habari za jeshi la polisi kuandikwa kwenye vyombo vya habari kutokana na tukio hilo kwa kuwa kazi ya vyombo vya habari mojawapo ni kuwatumikia wananchi hivyo kwa kufanya hivyo ni kuwanyima wananchi haki yao ya kupata taarifa.

Wakati huo huo, mwandishi wa habari mwandamizi, Saed Kubenea, amefichua njama zinazoratibiwa na Idara ya Habari Maelezo za kutaka kulifungia gazeti la kila siku la Nipashe, linalomilikiwa na kampuni ya magazeti ya The Guardian Limited.

Kubenea amefichua mpango huo leo, wakati akitoa tamko kulaani kitendo cha jeshi la Polisi kuwapiga na kufafanua kuwa Nipashe inataka kufungiwa isichapishe habari kwa sababu na mbinu zile zile za kunyamazisha vyombo vya habari, mbinu zilizotumika kuyafungia magazeti mengine ikiwemo Mwanahalisi, Mwananchi na Mtanzania.

Kwa upande wake, rais wa Klabu za Waandishi wa Habari Kenneth Simbaya amelaani tukio la kupigwa waandishi wa habari ambapo amesema jeshi la polisi halikuwa na sababu ya kutumia nguvu kubwa kiasi kile kwani tofauti kati yake na waandishi wa habari zingeweza kumalizwa kwa mazungumzo kwani wote walikuwa wanatekeleza jukumu la kuwatumikia Watanzania.