Jumatano , 3rd Dec , 2014

Serikali imeombwa kutowafumbia macho viongozi na watendaji wanaotoa lugha za kejeli kwa wananchi na kuwakatisha tamaa na kuwadharau watanzania wenye mitaji midogo kuwa fedha zao ni vijisenti vya kununulia juisi

Serikali imeombwa kutowafumbia macho viongozi na watendaji wanaotoa lugha za kejeli kwa wananchi na kuwakatisha tamaa na kuwadharau watanzania wenye mitaji midogo kuwa fedha zao ni vijisenti vya kununulia juisi kwani viongozi wanaowadharau watu wanaowatumikia ni wazi kuwa hawawezi kusaidia.

Changamoto hiyo imetolewa na wafanyabiashara wadogo wa madini jijini Arusha ambao pamoja na kulipongeza bunge kwa kuonesha nia ya dhati ya kutetea wanyonge wameliomba kutupia macho rasilimali za asili yakiwemo madini ya Tanzanite waliyodai kuwa hayajasaidia kuwapunguzia watanzania umasikini kutokana na utendaji mbaya wa baadhi ya viongozi.

kiongozi wa wajasiriamali hao Bw. Laurent Edward amesema inasikitisha na ni vigumu kuamini kuwa pamoja na matatizo mengi yanayowakabili watanzania baadhi ya viongozi na watendaji wanagawana mabilioni ya fedha ambazo hawajazitolea jasho huku wananchi wa kipato cha chini wakiendelea kutaabika.

Aidha katika hatua nyingine kiongozi wa wananchi hao akiwemo Bw, Laurent Edward, lazaro Sangeti na Godluck Okeyo wamemuomba Mh Rais Jakaya Kikwete kuwa macho katika kushughulikia na kuchukua hatua juu ya sula la Escrow ili kuhakikisha kuwa baadhi ya watu hawatumii nafasi hiyo kuwachafua watendaji wasio na hatia.