Jumatano , 21st Sep , 2022

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro, imewahukumu watu watatu kati ya tisa waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya Ofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), anayefahamika kwa jina la Leonard Enyimba Yamakwa kwa makusudi.

Vijana watatu waliohukumiwa kunyongwa

Wauaji hao baada ya kumuua Mwanajeshi huyo walimbaka mpenzi wake akiwa juu ya mwili wa marehemu na kisha kutoweka na pikipiki na simu ya mwanajeshi huyo.

Msajili wa Mahakama ya Rufani, Selvester Kahinda amesoma hukumu hiyo na kusema Mahakama imejiridhisha pasipo kuwa na shaka lolote kuwa watu hao ambao ni Charles Expedito, Hassan Athuman na Alfredy Dotto walimuua marehemu kwa makusudi hivyo adhabu yao ni kufa kwa kunyongwa.

Kahinda amesema awali kesi hiyo  namba 6 ya mwaka 2020 na kwamba kosa hilo lilifanyika Mei 25, 2019 majira ya saa 12:00 jioni eneo mashamba ya mkonge Tungi, Manispaa ya Morogoro.

Amesema kesi hiyo inawahusisha washtakiwa tisa na kati yao sita wameachiwa huru kwa sababu upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha kama kulikuwa na nia ya pamoja ya kutenda kosa la mauaji.

Hivyo kwa kukosekana kwa uthibitisho wa uhusika kwa washtakiwa namba nne hadi tisa waliachiwa huru ambao ni Juma Saidi, Yusuph Saidi, Mbaya Edward, Mnambo Maiko, Rehema Kibwana na Daudi Chilogo.