Vichwa 15 vya treni kununuliwa na serikali

Friday , 13th Oct , 2017

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeunda tume ya watu 11 kuchunguza vichwa 15 vya treni ambavyo Rais Magufuli alivikuta bandarini vikiwa havina mwenyewe mwanzoni mwezi Julai, 2017 ili kama vitathibitika kuwa ni vizima serikali ivinunue.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema hayo leo jijini Dar es Salaam na kusema kuwa serikali imekusudia kuvinunua vichwa hivyo vya treni kwa matumizi endapo vitakuwa ni vizima na kama havitakuwa na matatizo yoyote. 

Prof. Makame amesema endapo vichwa hivyo vikionekana ni vizima kwa mujibu wa uchunguzi  ukaofanywa na tume hiyo ya watu 11 iliyoundwa na serikali  hivyo serikali itakaa chini na mmiliki wa vichwa hivyo 15 vya treni na kuzungumza naye biashara.  

"Bila ya kuwa na treni za kutosha na vichwa vya kutosha hatuwezi kuhudumia mizgo yote inayopita bandari ya Dar es Salaam, kwa kulitambua hilo serikali tukaona ipo haja kufanya tathimini juu ya vichwa vile maana tuna wataalam wazuri wako pale wanaangalia ubora wa mashine, wanaangalia umeme wa vichwa vile baada ya hapo tukijiridha tutakaa pamoja na yule aliyeleta vichwa vile tuzungumze tupate 'Win to win situation' sisi tuwe tumefaidika na wao wawe wamefaidika ndiyo nia ya serikali" alisema Waziri Makame Mbarawa  

Mwezi Julai Rais Magufuli alipokuwa akiweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam alisema ameviona vichwa vya treni zaidi ya 15 ambavyo kwa muda huo vilikuwa vinaonekana havina mmiliki, na kudai kuwa vichwa hivyo vya treni ni vibovu. Rais aliagiza Wizara husika kulifanyia kazi jambo hilo ili ukweli ufahamike kuhusu vichwa hivcyo 15 vya treni.